WIKI iliyopita kwenye safu hii ya Funguka na Risasi tulikuwa naye mwigizaji Jacqueline Pentzel ‘Jack wa Chuz’ ambaye alifungukia ndoa yake na kashfa yake ya kujiuza.
Funguka: Mambo vipi Fid Q?
Fid Q: Poa, niaje?
Funguka: Bila shaka umezipata habari za kifo cha Bi. Kidude, wewe binafsi ulizipokeaje taarifa hizo?
Fid Q: Dah! Kwanza mimi niseme kuwa binafsi nimepata pigo kubwa na siyo mimi peke yangu bali Watanzania wote.
Funguka: Unadhani ni kwa nini msiba unawagusa Watanzania wote?
Fid Q: Bi. Kidude alikuwa na hadhi ambayo kila msanii angependa kuifikia. Ilifika hatua kwamba hata watalii waliokuwa wanakuja Bongo, walipitia Zanzibar kuangalia vivutio mbalimbali ikiwemo kumuangalia Bi. Kidude ambaye alikuwa akiwavuta watu wengi.
Funguka: Wewe ni mmoja wa wasanii wachache wa kizazi kipya waliowahi kufanya kazi naye, unamzungumziaje, alikuwa ni mtu wa aina gani?
Fid Q: Bibi Kidude alikuwa ni mtu ambaye kwanza, alikuwa amebarikiwa kwa kipaji na umri mkubwa ambao hata ndugu zake wenyewe hawakuwa wakiufahamu vizuri. Binafsi ninamfahamu kama kiongozi kwa wasanii na mara nyingi alikuwa hasiti kumrekebisha mtu akikosea.
Funguka: Tunavyojua marehemu alikuwa mtu adimu sana kupatikana hasa kutokana na shoo na ziara mbalimbali, wewe ulimpataje ukamshawishi ufanye naye kazi?
Fid Q: Kweli, marehemu alikuwa bize sana. Mara nyingi alikuwa akienda Uarabuni na Ulaya. Nilianza kumtafuta kuanzia mwaka 2006, lakini nikafanikiwa kufanya naye kazi mwaka 2008 tena kwa msaada wa watu wa karibu waliokuwa wakimfahamu.
Funguka: Wimbo uliofanya naye unaitwaje?
Fid Q: Wimbo unaitwa Juhudi za Wasiojiweza ulikuwa na ladha flani hivi tofauti na ngoma zangu nyingine zilizozoeleka.
Funguka: Sasa ni nini ambacho wewe binafsi au na wasanii wenzako mmepanga mkifanye ili kumuenzi marehemu?
Fid Q: Kwa sasa (Aprili 17) nipo Zanzibar msibani, lakini baada ya shughuli nzima za mazishi kuisha, nina imani mawazo mbalimbali yataanza kuibuka kuhusu nini cha kufanya ili kumuenzi marehemu?
Funguka: Tunashukuru kaka.
Fid Q: Poapoa haina noma.
0 comments:
Post a Comment