Wiki
iliyopita, nilieleza kuwa kama marafiki wenyewe wanachukuliana wapenzi,
ni kwa nini isikupe sababu ya kuamini kwamba wewe upo sahihi zaidi
kwenye uamuzi wako kuliko mshauri? Pengine anakujaza maneno ya chuki kwa mwenzi wako, mwisho ukamwona hafai, baada ya majuma mawili unagundua yupo naye.
Ukiweka
pembeni hoja ya kuchukuliana wapenzi, ukweli mwingine ni kwamba rafiki
anaweza kukufanya uachane na mwenzi wako mnayependana na kuelewana
vizuri ili ukajiweke kwa mwenye fedha. Mwisho wa hilo siku zote kuna
majuto, kwa maana pesa itakuwezesha kutatua mambo mengi lakini haziwezi
kukupa penzi linalokidhi moyo.
Kama ambavyo umewahi kushuhudia mateso
ya mtu kulazimishwa kuoa au kuolewa na yule asiyempenda kwa sababu
mbalimbali, hususan kichocheo cha shinikizo la wazazi, ndivyo hutokea
pale uhusiano unapojengwa na fedha. Shika neno hili kuwa binadamu ni
rahisi sana kuzizoea fedha pale anapokuwa anazipata.
Anapozoea maisha
ya fedha, moja kwa moja humuona wa kawaida sana, yule mwenzi wake
aliyemkubali kwa sababu ya mali. Ni hapo ndipo humsaka yule atakayempa
tulizo la kweli la moyo. Vitendo vya wenye fedha wengi kusalitiwa, ikupe
sababu ya kuyazingatia haya.
Kwa nini baadaye uje kuvuna aibu ya
kuonekana msaliti? Amua leo kwamba pamoja na hali yoyote ya kimaisha
uliyonayo na mwenzi wako, mtalindana kwa shida na raha. Yote
yanawezekana, endapo kwa maelewano yenu na nia ya dhati, mtajitolea
kusaka maisha bora zaidi, yatapatikana tu.
Epuka kukimbilia mali
zilizotafutwa na mwingine kisha wewe uje uvune tu. Wengi wamenyanyasika
sana na matokeo yake wakaishi maisha ya mpenzi wa picha. Yaani,
akimkumbuka labda aangalie picha, vinginevyo muda mwingi anakuwa ‘bize’
na kazi au na wapenzi wengine ambao ataona wanaendana na wakati.
Wewe
alikuona unafaa kwa wakati wako, jeuri yake ya fedha inamfanya atafute
wengine ambao ataona wanamtosheleza kutokana na wakati wao. Inawezekana
akakuacha au akaamua kukufanya mpenzi wa mapozeo. Yaani siku nanga
zikipaa, anakuja kwako umpe joto, akishatosheka na kukupa kisogo,
humuoni tena mpaka baada ya miezi mitatu.
Linda penzi lako. Kwa hali
yoyote aliyonayo mwenzi wako, unatakiwa kuhimili vishindo vya aina zote.
Fedha na vishawishi vya marafiki, wewe achana navyo. Hapa namaanisha
jinsia zote, kwani ipo mifano mingi ya wanaume kuwaacha wenzi wao na
kukimbilia kwa wanawake wenye fedha au kutokana na maneno ya marafiki.
Acha
tamaa, tunza moyo wako; dhana ya mashindano katika mapenzi ni muhimu
sana. Itakupa sababu ya kupigana kwa akili bila kutumia nguvu,
kuhakikisha unakuwa bora. Husika kikamilifu mpaka mwenzi wako akiri
kwamba hajawahi kuyafurahia mapenzi kama anavyofurahia akiwa na wewe.
Ni
muhimu tu kujua kwamba marafiki hawawezi kuwa kila kitu kwenye maisha
yako ya kimapenzi. Endapo utawaendekeza, wao ndiyo watakaokuwa wa kwanza
kuupeleka kaburini uhusiano wako wa kimapenzi. Sasa hapo unaweza kuamua
mwenyewe, kujenga au kubomoa.
0 comments:
Post a Comment