Written By warrior on Sunday, April 28, 2013 | Sunday, April 28, 2013
TUKIO la kukamatwa na kuwekwa
mahabusu kwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), kwa madai
ya uchochezi, limeibua sura mpya baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kutajwa kuwa nyuma ya mkakati huo,
Lema ambaye bado anaendelea kusota rumande siku ya tatu baada ya kunyimwa dhamana,ameanza kufanyiwa vituko na Jeshi la Polisi baada ya jana asubuhi mkewe kuzuiliwa asimpe mswaki wala chai.
Mbunge huyo alikamatwa kutokana
na amri ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, aliyedai kuwa
aliwachochea wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha kumzomea kiongozi huyo
na kupopoa gari lake kwa mawe.
Hata hivyo, siku moja kabla ya
kukamatwa Lema aliwaonesha waandishi wa habari ujumbe mfupi wa simu ya
kiganjani aliyotumiwa na Mulongo akimtishia kuwa atamfungulia kesi
yoyote anayoitaka.
“Umeruka kihunzi cha kwanza, nitakuonesha kuwa mimi ni serikali, ulikojificha nitakupata na nitakupa kesi ninayotaka mimi,’’ulisomeka ujumbe huo uliotumwa kupitia simu namba0752 960276ambayo Lema alidai ni ya Mulungo.
Pia nguvu kubwa iliyotumika
kumkamata mbunge huyo usiku saa 5:30 kwa kutumia askari na maofisa wa
usalama kuzingira nyumba yake, imehojiwa na baadhi ya wananchi,
wakitilia shaka kuwa kuna siri ndani yake.
Madai ya Mulongo kuwa Lema
alichochea wanafunzi hao yanakinzana na ushahidi wa video unaoonesha
kuwa mbunge huyo alitumia kila aina ya ushawishi kuwasihi wasiandamane
baada ya mwenzao, Elly Kago (22), kuuawa na watu wasiojulikana jirani na
chuo hicho.
Akizungumza na gazeti hili jana, mke wa Lema, Neema, alisema kuwa alifika kituo cha polisi asubuhi akipeleka chai, lakiniakaelezwa kuwa haruhusiwi kumpelekea chai.
Alisema kuwa alipiga simu kwa mkuu wa upelelezi wa mkoa ndipo akaambiwa ampelekee na alipofika tena kituoniaskari aliyekuwa zamu alianza kupekua mfuko wa Neema kwa fimbo, kisha akaamuru Lema apewe, ila anywe kwa dakika tatu.
Wakati anafungua chupa ya chai na kumimina kwenye kikombe,askari alimweleza kuwa imebaki dakika moja,hatua iliyomuudhi Lema akidai ni udhalilishaji, hivyo akashindwa kunywa.
Alipotaka kupewa mswaki,askari alikataa kuwa vifaa hivyo vinaweza kutumika kama silaha, hivyo haruhusiwi kupewa.
Tanzania Daima Jumapili
lilizungumza na wanasheria kadhaa pamoja na wanasiasa wabobezi kuhusu
sakata hilo, ambapo baadhi walidai huo ni mkakati wa CCM kutaka
kuidhoofisha CHADEMA katika uchaguzi mdogo wa madiwani ujao kwenye kata
nne.
“Kesho mnaweza kusikia Lema
akifunguliwa kesi ya ajabu ya kutunga halafu kwa kipindi hiki kampeni
zikianza mahakama itakuwa ikiisikiliza mfululizo ili asipate nafasi ya
kushiriki kikamilifu.
“Huu mkakati si wa Mulongo peke
yake bali ni mbinu za CCM zilizobakia katika kuhakikisha wanaikamata
Arusha. Lakini naona kama wanazidi kujimaliza,” alisema mwanasiasa mmoja
aliyeomba kuhifadhiwa jina lake.
Mwanasiasa huyo kutoka mkoani
Arusha aligusia pia mkanganyiko wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hivi
karibuni kutangaza kata nne kurudia uchaguzi na kuiacha moja ya
Sombetini ambayo diwani wa CCM alihamia CHADEMA.
“Ujue CCM wanafanya mambo bila
kupima athari, Arusha ni mji wa kitalii lakini kwa sasa unaogopeka kwa
fujo za polisi na wanasiasa, hata kesho utaona wakati Lema akipelekwa
mahakamani.
“Hapa ni ngome ya CHADEMA hata
kama Lema hayupo, sasa NEC wameibana Sombetini kwa hofu kuwa kata zote
zikienda CHADEMA watakuwa na madiwani zaidi ya CCM, hivyo ishu ya meya
kufufuka upya, ndiyo wakaamua kumtumia Mulongo kufanya mchezo huu wa
hatari,” alisema.
Alipopigiwa simu jana jioni na kuulizwa juu ya madai hayo, Mulongo alizungumza kwa ukali akisema:“Wewe mhariri unaweza kunipigia simu kuniuliza swali kama hilo?”..
Aliendelea kufoka akisema: “Acheni kufanya kila kitu siasa, wewe ni polisi kujua Lema kwanini akamatwe hivyo, niache mimi niko na wageni wangu,” alisema na kukata simu.
Mwenyekiti wa Chama cha
Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Francis Stolla, alizungumzia suala la
kukamatwa kwa Lema akisema kuwa nguvu kubwa na utaratibu uliotumika
kumkamata haukuwa wa busara.
Stolla alisema: “Kwa mujibu wa
kifungu cha 58 na 59 vya sheria ya ushahidi, Jeshi la Polisi au hata
kama ni kwa amri ya mkuu wa mkoa ya kukamata walipaswa kuchagua njia
nyingine ya busara.
“Jeshi linaweza kuwa na mamlaka
mapana ya kukamata au hata kama ni kwa amri ya mahakama, busara
huhitajika kutumika. Lema ni mbunge, anafahamika na upatikanaji wake
hauna utata, anapotuhumiwa kuhitajika polisi busara inatumika kumwita au
kumwandikia aende, si kumvizia kama walivyofanya,” alisema.
Mwanasheria mwingine ambaye
aliomba kuhifadhiwa jina, alifafanua kuwa: “Rais peke yake ndiye Amiri
Jeshi. Uamiri jeshi wa rais haugawanyiki mpaka kwa wakuu wa mikoa.
“Uamiri jeshi wa rais upo
kikatiba, hauwezi kuwa wa wakuu wa mikoa au wa wilaya. Ndiyo maana
anayeamrisha polisi katika mkoa ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa, na
wilayani anakuwapo ofisa anayeamrisha (OCD),” alisema.
Aliongeza kuwa sheria zinaruhusu
mkuu wa mkoa na wilaya kutoa amri ya kukamata mtu kama hakuna askari
lakini mtuhumiwa anapokamatwa sharti aambiwe anakamatwa kwa kosa lipi na
anayemkamata ajitambulishe.
Alisema kuwa siku ya tukio
chuoni, polisi walikuwapo wakati Lema akizungumza na wanafunzi na
hawakuona kosa lolote kwake ndiyo maana hawakumkamata, sasa iweje mkuu
wa mkoa aje na amri.
Akizungumzia nguvu iliyotumika
katika kumkamata Lema, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA)
Mkoa wa Tanga, Aaron Mashuve, aliliomba Jeshi la Polisi kuelekeza nguvu
kama hizo katika kusaidia watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).
Alisema nguvu hiyo kama
ingetumika wauaji hao wangekuwa wamekamatwa badala ya polisi kupoteza
muda kuhangaika na wanasiasa ambao wanaweza hata kuitwa kituoni wakaenda
kwa hiari yao.
Katika hatua nyingine, CHADEMA
mkoani Arusha kimetangaza kumfungulia mashtaka mkuu wa mkoa huo kwa
tuhuma za kumtishia mbunge wao kwa ujumbe wa maandishi, pia kumtaka
athibitishe madai ya kuwa kifo cha mwanafunzi kina uhusiano na masuala
ya kisiasa.
Katibu wa mkoa wa chama hicho,
Amani Golugwa, alisema taratibu za kuyashughulikia masuala hayo yote
mawili zinaendelea chini ya jopo la wanasheria wa chama hicho
0 comments:
Post a Comment